Thursday, June 23, 2011

Kabwe Zitto, Mwanasheria Mkuu hapakutosha


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe jana aliibua vuta nikuvute na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema katika kikao cha bunge kinachoendelea.

Zitto alikuwa mbongo na kumtaka Jaji Werema afute kauli yake aliyotamka “Kuna watu wanajenga hoja kwa sababu wanaonekana kwenye televisheni.”

Jaji Werema alimjibu Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wakati akichangia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya kodi katika kipindi ambacho bunge zima lilikaa kamati nzima chini ya Mwenyekiti Anne Makinda (Spika wa Bunge).

Baada ya Werema kutamka maneno hayo, Zitto alisimama na kumtaka afute kauli yake kisha aliongeza: “Nafikiri Werema alikuwa anaumwa, hivyo hayupo sawasawa.”

Zitto aliongeza: “Maneno ya Werema hayafanani na mtu ambaye amesomeshwa kwa fedha za wananchi maskini.”
Baada ya kauli hiyo, Spika Makinda alisema: “Naomba Mwanasheria Mkuu ufute kauli yako.”

Jaji Werema aliposimama hakufuta kauli yake isipokuwa alikanusha kauli ya Zitto iliyodai alikuwa anaumwa kwa hiyo hayupo sawaswa.

Zitto alisimama na kufuta kauli yake lakini Makinda alimkomalia Werema afute kauli yake, mwisho alisimama na kuondoa kauli hiyo aliyodai Lissu alizungumza hoja yake kwa lengo la kuonekana kwenye televisheni.

HOJA YA LISSU
Alitaka sheria inayomruhusu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa msamaha wa adhabu ya kodi iondolewe kwa sababu inatoa mianya ya ufisadi.

Hata hivyo, kura ilipopigwa, mapendekezo hayo ya Lissu yalishindwa kwa sababu wabunge wote wa CCM walipinga, huku wabunge wa upinzani walitaka hoja ya Lissu ipite.


CHANZO: Global Publishers Tz

No comments:

Post a Comment