JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lililazimika kuimarisha ulinzi katika Kituo chake Kikuu (Central) na baadhi ya maeneo ya jiji kukabiliana na tishio la wanachama wa Chadema kuandamana ili kushinikiza Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe aliyekamatwa juzi aachiwe.
Mbowe ambaye alikamatwa juzi ikiwa ni kutekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyoamuru akamatwe popote alipo na afikishwe hapo kwa kutotii amri ya kufika mahakamani katika kesi inayomkabili, alitarajiwa kupelekwa huko wakati wowote kuanzia jana akiwa chini ya ulinzi.
Jana, vijana wa Chadema walikusanyika katika kituo hicho huku wakilaani kitendo cha kukamatwa kwa mwenyekiti wao huku wengine wakijikusanya katika vikundi vidogovidogo katika maeneo mbalimbali katika Barabara za Morogoro na Nyerere, lengo likiwa kushinikiza kiongozi huyo atolewe rumande na asisafirishwe kupelekwa Arusha.
Taarifa kutoka Arusha ambako kesi ya kiongozi huyo inatarajiwa kuendelea leo asubuhi zinaeleza kuwa polisi jana jioni waliendesha msako wa wanachama wa Chadema waliokuwa wakihamasishana kuhudhuria kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha.
Wanachama na mashabiki hao wa Chadema walidai kwamba kitendo cha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni ni mpango uliobuniwa na CCM wa kubinya demokrasia ya vyama vingi nchini.
Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Zitto Kabwe walikamatwa katika maeneo tofauti nchini juzi. Wakati Mbowe alidaiwa kutotii amri ya mahakama, Zitto alidaiwa kuzidisha muda wakati wa kuhutubia mkutano wa hadhara mkoani Singida.
“Tumeongea na polisi, bado wanamng'ang'ania Mbowe. Msimamo wao ni kumpeleka Arusha, tuangalie utaratibu utakaotumika katika kumsafirisha,” alisema Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika.
Baada ya kauli hiyo ya Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubunge, vijana wa chama hicho wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob walianza kuimba nyimbo za kulaani kukamatwa kwa mwenyekiti wao huku wakisema muziki wa Chadema polisi hawauwezi.
Ofisa mmoja mwadamizi wa Polisi Ilala ambaye hakujitambulisha jina aliwaambia vijana hao kuwa polisi na walishakubaliana na viongozi wa Chadema kuwa mtuhumiwa huyo amepangiwa utaratibu wa kusafirishwa kwenda Arusha kuhudhuria kesi yake.Ofisa huyo aliwataka wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo kuondoka ili kupisha jeshi hilo kuendelea na kazi ya kutoa huduma kwa watu wengine.
“Tumeshaongeza na wakubwa wenu, hiki ni kituo cha polisi watu mbalimbali wanakuja kupata huduma hapa. Mtu haji kuangaliwa kwa aina hii ya hamasa na nyimbo, tunaomba muondoke,” alisema ofisa huyo.Kauli hiyo ilipingwa na vijana hao wakisema ofisa huyo ni mtu wa kawaida hawezi kuwaeleza mambo kama hayo.
“Sisi hapa tuna viongozi wetu mambo kama hayo tungeelezwa na kuelewa kama yangesemwa nao na si mtu wa kawaida kama wewe,”alisikika mmoja wa wanachama hao akisema kwa sauti.
Kauli hiyo ilimshangaza ofisa mwingine wa polisi aliyeibuka na kuhoji: “Mnasema huyu ni mtu wa kawaida? Akajibiwa “ndiyo”, “huyo siyo mtu wa kawaida."Vijana hao waliendelea na msimamo wao: “Sisi tunasema huyo ni mtu wa kawaida kwa sababu siyo kiongozi wetu, ndiyo maana tunasema angekuwa kiongozi wetu tungemwelewa.”
Kauli hiyo ilimlazimisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile kujitokeza na kuwataka watu hao kuondoka katika eneo hilo kwa sababu kulikuwa na shughuli mbalimbali zilizokuwa zikiendelea.
“Tumeongea na viongozi wenu, tumeshakubaliana tunawaomba mtawanyike na sisi tuendelee na kazi, sitaki mkusanyiko wowote katika kituo cha polisi,” alisema Shilogile.Mara baada ya kauli hiyo gari la maji ya kuwasha lilianza kusogea walipokuwa wafuasi hao wa Chadema likitanguliwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia waliokuwa wakiwafukuza katika eneo hilo.
Kundi hilo liliondoka na kuelekea makao makuu ya Chadema ambako Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alikuwa na mkutano na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment