Tuesday, June 21, 2011

AJILIPUA NA MWANAYE BAADA YA KULETEWA MKE MWENZA

Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Monica Barthelemeo mkazi wa Mabibo Makuburi jijini Dar es Salaam, amejilipua kwa kiberiti na mwanaye aitwae Anastazia Leonard baada ya kudai kuletewa mke mwenza na mumewe aliyetajwa kwa jina la Leonard.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa Juni 12, mwaka huu maeneo ya Mabibo External jijini baada ya mwanamke huyo kujimwagia mafuta ya taa pamoja na mwanaye kisha kujilipua kwa kiberiti.

Akizungumzia tukio hilo, dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Godriver Barthelemeo alisema marehemu kabla ya kifo chake alikuwa akiishi mkoani Geita kama mke wa Leonard na kufanikiwa kupata watoto wawili, Anastazia (3) na Edward (5), lakini siku za hivi karibuni kuliibuka mizozo ya kimapenzi baina yao.

Alisema mizozo hiyo ilianza ambapo marehemu alikuwa akimtuhumu mumewe kulala nje mara kwa mara bila taarifa yoyote na akadai baadaye mume huyo alimpeleka mwanamke mwingine ndani ya chumba walichokuwa wakiishi na yeye pamoja na watoto kufukuzwa.

“Baada ya kufukuzwa marehemu na watoto wake walifunga safari na kuja hapa Dar na kufikia kwangu Mabibo Makuburi, akanisimulia mkasa wa kufukuzwa na mumewe na kuletewa mke mwenza,” alidai Godriver.

Aliongeza kuwa baada ya kusikiliza kilio cha mdogo wake aliahidi kumpa ushirikiano lakini marehemu alionekana kuchanganyikiwa kutokana na tukio hilo na kuanza kufanya mambo yasiyoeleweka ikiwemo kuongea peke yake.

Alisema Juni 12, mwaka huu akiwa nyumbani alifuatwa na kijana mmoja na kupewa taarifa kuwa ndugu yake amejimwagia mafuta ya taa na kujilipua pamoja na mwanaye.

Kufuatia tukio hilo wasamaria walimkimbiza Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam lakini kutokana na hali zao kuwa mbaya walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Madaktari walijaribu kuokoa roho za majeruhi hao lakini mtoto aliaga dunia Juni 15, mwaka huu na mwanamke huyo alifariki dunia siku mbili baadaye.

Marehemu alitarajiwa kuzikwa jana (Jumatatu) katika Makaburi ya Mabibo jijini Dar.



Source: Global Publishers Tz
http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/ajilipua-na-mwanaye

No comments:

Post a Comment